GABO: TARATIBU UNAUKATAA UFALME WA BONGO MOVIE.
GABO: TARATIBU UNAUKATAA UFALME WA BONGO MOVIE.
Na Mwinjuma Kimaya
Wakati tunaelekea kutimiza miaka 5 toka kutokea kifo cha mwigizaji nguli wa filamu za kitanzania mwigizaji Steven Charles Kanumba......bado tasnia ya filamu ilionekana ni yenye kuchechemea na kujikongoja. Hii ilipelekea mpaka watu tukaamini kuwa Kanumba ameondoka na bongo movie yeka.
Hakuna asiyejua uwezo aliokuwa nao Kanumba kwenye kuigiza na kuongoza filamu, hakuna asiyetambua kipaji cha Kanumba kwenye kukonga nyoyo za wapenzi wake ila alipoondoka ndipo tulipojua thamani ya kipaji chake.
wakati watanzania wana majonzi na masikitiko makubwa juu ya kuanguka kwa kiwanda hiki cha filamu yaani Bongo Movie ndipo jina la Salim Ahmed Issa almaalufu Gabo Zigamba likaibuka na kutenda kile wapenzi wa filamu walikosa kwa muda. Ukiachilia mbali uwezo wake wa kuigiza kwa hisia kipande chochote utakachompa, achana na uwezo wake wa kuigiza sauti za watu wa kaskazini mwa Tanzania pamoja na sauti za watu wa kusini kule, bado ni muongozaji mzuri wa filamu, vile vile amekuwa ni mtangazaji wa kipindi cha Bondeni kama kinavyorushwa na TBC1.
Ukifatilia kwa makini filamu alizocheza au kuongoza kuna kitu utakiona kuwa kimerudi, kuna radha unaiona imeongezeka ndani ya filamu alizoshiriki, angalia filamu kama 007 Days, The Killer, Safari, Fikra zangu, Kona kisha angalia Safari ya Gwalu utajua naongelea nini hapa.
Gabo sio tu amekuwa msanii wa filamu bora kwa miaka miwili mfululizo bali ndo ameibeba bongo movies kwa sasa mara baada Rey, JB na Dr Cheni, Tino, Wolper, Wema Sepetu na akina Hemedi Phd kuwa kimya na kujikita kwenye mambo yao.
Pamoja na uwezo alonao Gabo, pamoja na kipaji alichonacho msanii huyu bado nafikiri hajajua nguvu yake pamoja na matakwa ya watanzania kwenye tasnia ya filamu. Wakati watanzania wakiitaji zaidi filamu ambazo zina ubora, stori za kipekee na sio kila siku mapenzi, ubunifu pamoja na mchanganyiko wa ladha yaani kushirikisha wasanii wa nje ya mipaka ya Tanzania bado Gabo amelala na kuwa bize kutengeneza filamu zile zile ambazo tumeshazoea.
Kwangu mimi ufalme wa bongo movie upo wazi kwa Gabo Zigamba, Watanzania tumeshaamua kumsimika yeye kuwa mrithi wa Kanumba hivyo anapaswa kujifunza kwa kile alichofanya Steve na ikiwezakana afanye zaidi yake.
Kuendelea kuigiza filamu anazofanya sasa hivi ni kutowatendea haki Watanzania ambao wameamua kumuamini na kumtunuku hadhi ya mfalme wa filamu nchini. Gabo anza kuangalia nje ya Tanzania ni namna gani unaweza fanya ili kujitanua zaidi na kuleta ladha mpya ya filamu nchini, kisha ongeza ubunifu wa filamu zako.
Kuendelea kuigiza kama unavyoigiza sasa hivi kwa kuangalia zaidi ndani ya nchi bila kuwaza nje ya mipaka yetu ni KULIKATAA TAJI LA UFALME tulokupa na watanzania hawa watatafuta mtu wa kumpa muda si mrefu.
#Itaendelea
Mwinjuma Kimaya
0719 880514
No comments